MTUMISHI WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAKOSA YA RUSHWA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Chato mnamo tarehe 02/09/2016 ilimfikisha mahakamani Bw. MBARAKA MAULID MLAPONI ambaye ni Afisa Misitu msaidizi katika kituo cha Bwanga kwa makosa mawili ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007. Mshitakiwa huyo alisomewa mashitaka yake mbele ya hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Chato Mheshimiwa JOVITH KATO.

Akimsomea Mshitakiwa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chato, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bw. AUGUSTINO MTAKI aliieleza mahakama kuwa mnamo ya tarehe 21/8/2016 Mshitakiwa aliomba kiasi cha Tshs. 50,000/= kutoka kwa Mwananchi jina limehifadhiwa ili amrudishie baiskeli yake aliyoikamata kwa kosa la kupitisha mazao ya misitu katika eneo la kizuizi ambapo baiskeli haziruhusiwi kupita na mazao ya misitu, na kwamba mnamo tarehe 26/8/2016 alipokea kiasi cha Tshs. 30,000/= ikiwa ni sehemu ya fedha alizoomba kama rushwa ili amrudishie baiskeli yake Mwananchi huyo aliyoikamata ikipita katika eneo lililozuiliwa.

Baada ya kusomewa mashitaka Mshtakiwa alikana mashtaka yote dhidi yake, Mwendesha Mashitaka aliiambia mahakama kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo umekamilika na kuomba tarehe kwa ajili ya kumsomea Mshitakiwa maelezo yake ya awali.

Mahakama ilimpa Mshitakiwa masharti ya dhamana ambapo alitakiwa awe na Wadhamini wawili wanaoaminika ambao watasaini dhamana ya kiasi cha Tshs. 1,000,000/= kila mmoja.Hata hivyo Mshitakiwa hakuweza kutimiza masharti hayo hivyo alipelekwa rumande hadi tarehe 15/9/2016 kesi hii itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa. Kesi hii imefunguliwa na kusajiliwa kama Kesi ya Jinai Na. 278/2016.

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita Bw. Musa Chaulo ametoa shukrani kwa raia wema wanaotoa ushirikiano kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Aidha ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya Rushwa na kuwa na Uthubutu wa kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa wakati wowote wanapohisi au kuona vinatendeka ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Imetolewa na

Bw. Musa Chaulo - Kaimu Mkuu wa TAKUKURU (M) Geita

05/09/2016

 

Prosecution

SAKATA LA ESCROW: VIGOGO WA BOT, TRA, TANESCO, REA NA ARDHI WAPANDISHWA KIZIMBANI 11 Sep 2015

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, imewafikisha katika mahakama...

More detail
MAWAZIRI WAWILI WA ZAMANI WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA TISA 10 Sep 2015

  Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), wamehukumiwa...

More detail
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Songea anaswa kwa Rushwa 10 Sep 2015

Mnamo tarehe 03/03/2015 TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Mwanasheria wa Halmashauri...

More detail