Dk Hoseah achaguliwa kuongoza mapambano ya rushwa A.Mashariki

dr hoseah

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Dkt. Edward G. Hoseah, amechaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Rais wa Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (East African Association of Anti-Corruption Authorities- EAAACA).

Uchaguzi huo umefanyika Jumanne tarehe 29/09/2015 jijini Entebe – Uganda, katika Mkutano Mkuu wa 8 wa shirikisho hilo ulioanza leo.

Hii ni mara ya pili kwa Dkt Hoseah kuchaguliwa kushika wadhifa huo kwani yeye ndiye aliyekuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo lililoanzishwa mwaka 2007.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwake, Dkt Hoseah amesema katika kipindi cha uongozi wake kama Rais wa EAAACA (2015 -2017) atatoa kipaumbele katika kutekeleza yafuatayo:

  1. Kuweka mikakati michache inayotekelezeka ikiwemo kufanya tafiti za kuziba mianya ya rushwa katika mifumo mbalimbali ya Taasisi katika za nchi za Afrika Mashariki.
  2. Kuimarisha uhusiano kati ya Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki na kuongeza jitihada za kuhakikisha EAAACA inajumuishwa katika Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (East African Community).

Shirikisho hilo linalojumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, liliundwa rasmi Septemba 28, 2007, ambapo viongozi wa TAKUKURU (Tanzania), IG (Uganda) na KACC (Kenya) - ambao ndio waanzilishi, walisaini azimio la kuwa na Ushirikiano wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki.

Azimio hilo lilipewa jina la ‘AZIMIO LA KAMPALA’ na lilitamka kwamba:

  • Taasisi hizi zinarejea dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na kufanya kazi pamoja katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.
  • Taasisi hizi zinatambua kuwa rushwa inaweza kuharibu ufanisi wa kiutendaji wa jamii yoyote, inahatarisha demokrasia, ukuaji wa uchumi na utawala wa sheria. Kwa msingi huu, Taasisi hizi zinaendelea kutilia mkazo kuundwa kwa EAAACA kama jukwaa la kubadilishana taarifa, uzoefu na kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kuzuia na kupambana na rushwa katika sura zake zote.
  • Taasisi hizi zinatambua kuwa jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mtu katika kila jamii na kwamba mapambano haya yanahusisha ulinzi na uimarishaji wa maadili katika jamii zote.
  • Uamuzi wa kuingia katika makubaliano haya na kuundwa kwa Ushirikiano huu ni ishara ya kweli ya dhamira ya kila moja ya Taasisi hizi katika kutokomeza rushwa.

Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 8 wa EAAACA inasema ‘Uimarishaji wa jitihada za kuzuia na kupambana na Rushwa katika nchi za Afrika Mashariki' na mkutano ujao wa mwaka, umepangwa kufanyika Tanzania mwaka 2016.

 

Prosecution

SAKATA LA ESCROW: VIGOGO WA BOT, TRA, TANESCO, REA NA ARDHI WAPANDISHWA KIZIMBANI 11 Sep 2015

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, imewafikisha katika mahakama...

More detail
MAWAZIRI WAWILI WA ZAMANI WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA TISA 10 Sep 2015

  Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), wamehukumiwa...

More detail
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Songea anaswa kwa Rushwa 10 Sep 2015

Mnamo tarehe 03/03/2015 TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Mwanasheria wa Halmashauri...

More detail