TAFAKARI: Picha ya video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii yamfukuzisha kazi Askari Polisi

askari rushwa

Askari Polisi Koplo Anthony Temu akiwa barabarani siku ya tukio la kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa dereva.

Na Angela Mulanduzi, Dar es Salaam

Novemba 9 mwaka 2015 picha ya ‘video’ ilisambaa katika mitandao ya kijamiii ikimuonyesha Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani akiomba na kupokea rushwa kutoka kwa dereva wilayani Handeni, mkoa wa Tanga.

Vitendo vya rushwa kama hivi vinatokea katika maeneo mengi kila siku lakini baadhi ya wananchi hawana ujasiri wa kurekodi ‘video’ na kuwasilisha TAKUKURU au Polisi ushahidi wa aina hii unaoweza kusaidia kumtia hatian mtuhumiwa. Pia inawezekana wale wenye ujasiri huo hawajawahi kupata wazo la kurekodi matukio kama hayo. Ujasiri na ubunifu uliofanywa na mwananchi aliyerekodi na kusambaza ‘video’ hiyo ni mfano mzuri wa mwananchi kushiriki kutimiza wajibu wake wa kuzuia na kupambana na rushwa.

Askari aliyehusika katika tukio hilo ni wa kituo cha Polisi Kabuku wilayani Handeni Kikosi Cha Usalama Barabarani, Koplo Anthony Temu (46) mwenye namba F. 785 na amefukuzwa kazi na mwajiri wake. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, kufukuzwa kazi kwa askari huyo kumetokana na taarifa ya kuomba na kupokea rushwa iliyopatikana kupitia mitandao ya kijamii.

Kamanda Mwombeji alieleza pia kuwa mtuhumiwa huyo ameshakabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tanga pamoja na kielelezo ambacho ni ‘video’ iliyokuwa ikirushwa kwenye mitandao ya kijamii ili waendelee kumshughulikia kwa upande wa jinai kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Bw. Aidan Ndomba alipoulizwa kuhusu hatua walizochukua, alithibitisha kupokea vielelezo kutoka Jeshi la Polisi na alisema tayari mtuhumiwa alifikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Aidha, alisema uchunguzi unaendelea.

Bw.Ndomba ametoa wito kwa kila mtanzania kushirikiana na TAKUKURU katika jitihada hizi za kuzuia na kupambana na rushwa kwani athari zake zinamgusa kila mmoja bila kujali anayejihusisha na rushwa au la@.

 

Prosecution

SAKATA LA ESCROW: VIGOGO WA BOT, TRA, TANESCO, REA NA ARDHI WAPANDISHWA KIZIMBANI 11 Sep 2015

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, imewafikisha katika mahakama...

More detail
MAWAZIRI WAWILI WA ZAMANI WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA TISA 10 Sep 2015

  Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), wamehukumiwa...

More detail
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Songea anaswa kwa Rushwa 10 Sep 2015

Mnamo tarehe 03/03/2015 TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Mwanasheria wa Halmashauri...

More detail