JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

EAAACA (East African Association of Anti-Corruption Authorities)

CHIMBUKO LA EAAACA

EAAACA ni Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki ambalo ni huru, lisilo na malengo ya kupata faida na lisilona mrengo wa kisiasa. Shirikisho hili liliundwa tarehe 28Septemba, 2007 Kampala Uganda na kuzinduliwa rasmi tarehe 9Novemba,2007 Nairobi,Kenya baada ya katiba yake kusainiwa. Shirikisho hili lilianzishwa na mamlaka tatu za kupambana na rushwa ambazo ni  TAKUKURU (Tanzania), IG (Uganda) na KACC (Kenya) Wakati wa uanzishaji wa shirikisho viongozi wa mamalaka hizi walisaini azimio la kuwa na Ushirikiano wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki. Azimio hilo lilipewa jina la ‘AZIMIO LA KAMPALA’ na lilitamka kwamba:

 • Taasisi hizi zinarejea dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na kufanya kazi pamoja katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.
 • Taasisi hizi zinatambua kuwa rushwa inaweza kuharibu ufanisi wa kiutendaji wa jamii yoyote, inahatarisha demokrasia, ukuaji wa uchumi na utawala wa sheria. Kwa msingi huu, Taasisi hizi zinaendelea kutilia mkazo kuundwa kwa EAAACA kama jukwaa la kubadilishana taarifa, uzoefu na kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kuzuia na kupambana na rushwa katika sura zake zote.
 • Taasisi hizi zinatambua kuwa jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mtu katika kila jamii na kwamba mapambano haya yanahusisha ulinzi na uimarishaji wa maadili katika jamii zote.
 • Uamuzi wa kuingia katika makubaliano haya na kuundwa kwa Ushirikiano huu ni ishara ya kweli ya dhamira ya kila moja ya Taasisi hizi katika kutokomeza rushwa.

Kuundwa kwa EAAACA ni ishara ya wazi ya dhamira ya viongozi wakuu wa taasisi hizi katika kutekeleza kwa mafanikio jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa katika nchi zao. Hatua hii pia, kama inavyojieleza katika tamko hilo, inazidi kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kila mwanajamii na mataifa katika kukabiliana na tatizo la rushwa duniani.

UANACHAMA KATIKA SHIRIKISHO

Uanachama katika shirikisho uko wazi kwa Mamlaka zote za Kupambana na Rushwa zilizoko kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki na nchi zingine za Afrika Mashariki. Pia milango iko wazi kwa Taasisi zingine zenye malengo yanayofanana na EAAACA kuwa watazamaji baada ya kuomba na kukubaliwa uanachama na kamati tendaji ya EAAACA. Kwa hivi sasa uanachama katika EAAACA ni kama ifuatavyo:

 1. Kamisheni ya Maadili na Kupambana na Rushwa, Kenya
 2. Federal Ethics Anti-Corruption Commission, Ethiopia
 3. Inspection General State,  Djibouti
 4. Ofisi ya Ukaguzi wa Serikali, Uganda
 5. Office of the Ombudsman,  Rwanda
 6. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) , Tanzania
 7. Kamisheni ya Kupambana na Rushwa,  Sudan Kusini
 8. Brigedi maalumu ya Kupambana na Rushwa, Burundi

VYOMBO VYA EAAACA

EAAACA ina vyombo vitatu ambavyo ni :

 • Mkutano Mkuu wa Mwaka ambao ni chombo cha juu cha uongozi wa shirikisho ambacho kinahusisha wawakilishi wa mamlaka za kupambana na rushwa na wanachama wa heshima.
 • Kamati ya Utendaji ambacho ni chombo kinachohusika na uongozi na utawala wa shirikisho na inahusisha rais, Makamu wa rais, Katibu Mkuu, na Wakuu wa Mamlaka  husika kama wajumbe.Urais ni wa kupokezana kwa muda wa miaka miwili. Rais wa kwanza wa shirikisho alikuwa Dr Edward Hosea toka Tanzania .
 • Sekretariati ambayo  ni chombo kinachohusika  na  utalaam na utekelezaji  wa shughuli za kila siku za  shirikisho . Makao makuu yake yako Kampala, Uganda.Sekretariati inaongozwa na Katibu Mkuu ambaye huteuliwa na Kamati ya Utendaji ya EAAACA

MALENGO YA EAAACA

 1. Kuimarisha, Kusaidia, na kuratibu ushirikiano baina ya nchi wanachama ili kuwezesha uchukuaji wa hatua na maamuzi yenye tija katika kuzuia, kubaini, kuchunguza, kuadhibu, na kukomesha rushwa
 2. Kuwa na ushirikiano wa kisheria katika kubaini, kuchunguza, uendeshaji wa mashtaka, utambuzi, ufuatiliaji, uzuiaji, ukamataji, utaifishaji, urejeshaji wa mali, vyombo, au mapato yaliyopatikana kwa njia za rushwa.
 3. Kufanya utafiti katika taratibu na uvumbuzi mpya na mzuri  ili kuboresha na kuongeza ufanisi wa mamlaka za kupambana na rushwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuandaa mafunzo ya pamoja ya watumishi kwa manufaa ya watumishi.
 4. Kuhamasisha uelewa wa wananchi juu ya madhara ya rushwa na nafasi ya jamiii katika kuzuia na kupambana na rushwa.
 5. Kuwezesha urejeshaji wa mapato yaliyopatikana kwa njia za rushwa au utakatishaji wa pesa au utajiri haramu na ukamataji wa mali yoyote iwapo mshirika yeyote katika katiba hii ataomba
 6. Kuratibu na  kulinganisha sera na sheria kati ya nchi wanachama kwa lengo la kuzuia, kubaini, kuadhibu, na  kutokomeza  rushwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 7. Kushirikiana katika eneo la kulinda mashahidi na mfumo wa kulinda watoa taarifa.

Katiba ya EAAACA

Kipeperushi cha EAAACA