Klabu za Wapinga Rushwa Tunduma zahamasisha jamii kupambana na rushwa

Na Sarah Chodota.

Wanachama wa Klabu za Wapinga Rushwa katika Shule za Sekondari Mwl. Julius K. Nyerere, Tunduma, Jakaya M. Kikwete na Mpakani mkoani Songwe, wameonyesha uwezo wao wa kuandaa kazi mbalimbali za klabu. Kazi zilizoandaliwa na klabu hizo ni nyimbo, mashairi na michezo ya kuigiza yenye maudhui ya kudhibiti rushwa wakati wa tamasha la michezo lililokutanisha klabu hizo Aprili 6, 2016.

Akizungumza wakati wa kufungua tamasha hilo, afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa -TAKUKURU wilaya ya Tunduma, Bi. Sheila Mlemba alieleza kuwa lengo la kuandaa tamasha hilo ni kuwakutanisha wanachama wa klabu za wapinga rushwa kutoka shule mbalimbali za sekondari zilizoko katika mji wa Tunduma ili kufahamiana, kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za klabu na kufahamu changamoto zinazozikabili klabu zao na namna wanavyozitatua.

Tamasha hilo lilijumuisha mashindano mbalimbali ya uimbaji kwaya, mashairi, maigizo na mchezo wa kukimbia na gunia. Katika michezo hiyo Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari Jakaya M. Kikwete iling’ara zaidi kwa kushinda michezo mitatu ya kuimba, maigizo na kuvuta kamba. Aidha kwa mchezo wa kukimbia na gunia upande wa wavulana mwanachama wa klabu kutoka Shule ya Sekondari Mpakani, Amani George aliibuka mshindi na kwa upande wa wasichana, Tatu Hassani wa Shule ya Sekondari Mwl. Julius K. Nyerere aliibuka mshindi.

youth 1

Baadhi ya wanachama wa klabu ya wapinga rushwa kutoka Shule ya Sekondari ya Jakaya M. Kikwete wakionyesha igizo lenye maudhui ya rushwa wakati wa Tamasha la michezo. Klabu zingine zilizoshiriki katika tamasha hilo ni Shule ya Sekondari Mwl. Julius K. Nyerere, Tunduma, na Mpakani za mjini Tunduma .

Wanachama walioshiriki katika tamasha hilo walipata nafasi ya kuelezea maoni yao ambapo mwanachama kutoka Shule ya Sekondari Tunduma, Eud Elly alisema kuwa tamasha hilo limewapa fursa ya kufahamiana na kujifunza mambo mbalimbali kutoka katika klabu nyingine.

Naye Mwalimu mlezi wa Klabu ya Wapinga Rushwa kutoka Shule ya Sekondari Mwl. Julius K. Nyerere, Bw. Isaya Seme, kwa niaba ya walimu walezi walioshiriki tamasha hilo aliushukuru uongozi wa TAKUKURU wilaya ya Tunduma kwa kuandaa tamasha hilo na kuichagua shule yake kuwa mwenyeji. Pia Bw. Seme aliongeza kuwa tamasha hili ni chachu na hamasa kwa wanafunzi wasio wanachama hivyo aliiomba ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Tunduma kuangalia uwezekano wa kufanya tamasha la ina hii mara kwa mara.

Bi. Mlemba akitoa neno la shukrani kwa walimu na wanachama walioshiriki tamasha hilo alisema, “Tunawashukuru Walimu Wakuu wa shule zote zilizoshiriki katika tamasha hili kwa kukubali kuwaruhusu wanafunzi wao kuacha ratiba za masomo na kushiriki tamasha hili. Pia tunatoa shukrani kwa Walimu Walezi na wanachama wao kwa maandalizi waliyofanya ili kufanikisha tamasha hili”.

Aliongeza kuwa, kufanyika kwa tamasha hilo kumewapa fursa washiriki hao kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu rushwa na kutumia sanaa ya nyimbo, maigizo na mashairi kufikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wenzao na jamii inayowazunguka. Pia tamasha hili litawahamasisha wanafunzi wasio wanachama kujiunga na klabu hivyo kuongeza jeshi la kupambana dhidi ya vitendo vya rushwa.

youth 2

Wanachama wa klabu ya wapinga rushwa kutoka shule za sekondari za Mwl. Julius K. Nyerere, Tunduma, Jakaya M. Kikwete na Mpakani mjini Tunduma wakishiriki mbio za gunia katika tamasha la michezo lililozileta pamoja klabu hizo.

---------------------------------------------------------Mwisho--------------------------------------------------

Klabu za wapinga Rushwa Kigoma zashindanishwa

Jengo la TAKUKURU(M) wa Kigoma

Ofisi ya TAKUKURU Kigoma imeendesha shindano kwa Klabu za Wapinga Rushwa mkoani humo ili kuzifanya klabu ziweze kuwa zinajisimamia zenyewe na Ofisi iwe inahusika katika kuziimarisha. Shindano hilo lilihusisha upimaji wa kazi mbalimbali zilizofanywa na zinazofanywa na klabu hizo.

Lengo la kuanzisha shindano hilo ni kuwapa changamoto wana klabu katika swala zima la mapambano dhidi ya rushwa kwa nafasi yao na pia kuwajengea uwezo wa kuwa wabunifu, wawajibikaji na hatimaye kujitegemea katika kutekeleza malengo ya klabu zao.

Waliohusika katika shindano hili ni Shule za Sekondari sita zenye klabu za wapinga rushwa katika Manispaa ya kigoma. Uhai wa klabu ndiyo ulizingatiwa katika uchaguzi wa klabu zilizoshindanishwa kwa vigezo vifuatavyo;-

 • Idadi ya mashairi yaliyoandikwa na wana klabu na kuwasilishwa ofisini kwa kumbukumbu.
 • Idadi ya debate zilizoandaliwa na kufanywa na wana klabu zilizohusiana na mapambano dhidi ya rushwa na taarifa kuwasilishwa Ofisini,
 • Idadi ya vikao vilivyofanywa na wanaklabu kwa muda wa klabu wakiwa shuleni (mhutasari ya vikao hivyo)
 • Shughuli mbalimbali zinazofanywa na wana klabu hapo shuleni ambayo inaonesha uwepo wa uhai wa klabu. Shughuli hizo ni pamoja na kufanya usafi na kulima bustani.
 • Idadi ya siku walizopanga kwenda kutembelea klabu za shule jirani na kukaa kwa pamoja na kujadili maswala ya rushwa.
 • Idadi ya makala walizoandika na kuziwasilisha Ofisini
 • Uhai wa klabu husika kwa kuangalia wanachama waliojiandikisha awali na waliopo hadi sasa

  Katika shindano hilo, Majaji ambao ni Maafisa wa TAKUKURU waliandaa ‘check list’ kulingana na vigezo vilivyoshindanishwa na kwenda katika shule husika na kuona shughuli wazifanyazo kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa. Pia Majaji walihakiki mashairi na mada zilizowasilishwa ofisini kutoka katika klabu husika. Kila kigezo kilipewa alama kwa kutofautisha kati ya kigezo kimoja na kingine kulingana na umuhimu. Jumla ya alama zilikuwa ni asilimia mia moja (100%).

  Jumla ya washindi watatu walipatikana na kupatiwa zawadi zifuatazo:

  • Mshindi wa kwanza – Shule ya Sekondari Mwananchi alipata ngao na shilingi elfu hamsini tasilimu.
  • Mshindi wa pili – Shule ya Sekondari Katubuka alipata ngao na shilingi elfu arobaini tasilimu na
  • Mshindi wa tatu – Shule ya Sekondari Kigoma walipata ngao na shilingi elfu thelathini tasilimu. Vilevile, shule zote sita (Mwananchi, Katubuka, Kigoma, Lusimbi, Buteko na Kitwe) zilizoshiriki katika shindano hilo walipatiwa vyeti vya ushiriki.

  TAKUKURU ilianzisha utaratibu wa kuwa na Klabu za Wapinga Rushwa mwaka 2007 ambapo klabu hizio zilifunguliwa katika Shule za Msingi, Sekondari pamoja na Vyuo kwa malengo yafuatayo:

  • Kushirikisha jamii na hasa vijana katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa.
  • Kujenga maadili mema kwa watoto wakiwa na umri mdogo,
  • Kujenga uelewa wa athari za rushwa katika jamii na hii itawafanya kujua ubaya wa uwepo wa vitendo vya rushwa,
  • Kujenga ujasiri wa kukataa uwepo wa vitendo vya rushwa,
  • Kujenga uelewa wa kila mmoja kujitambua kuwa ana wajibu wa kupambana na vitendo vya rushwa pale alipo na si TAKUKURU pekee yake.
  TAKUKURU ina wajibu wa kufungua klabu za wapinga rushwa na kutoa elimu kuhusiana na rushwa na baada ya klabu kufunguliwa, walezi, viongozi wa klabu na wanachama wanapaswa kuhakikisha klabu hizo zinakuwa hai kwa kubuni na kufanya kazi mbalimbali zilizo ndani ya uwezo wa klabu husika. Hata hivyo baadhi ya klabu zinapofunguliwa huwa mfu kwa kutojishuhulisha au kubuni njia mbalimbali za kujielimisha katika swala zima la rushwa.

TAKUKURU YATOA SOMO KWA VIJANA NA WAJIBU WAO KATIKA KAMPENI NA UCHAGUZI MKUU

Na Faisal Abdul

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewakumbusha vijana nchini kuhusu umuhimu wa kutokubali rushwa ili kuchagua kiongozi.

Hayo yalielezwa katika Semina kwa vijana iliyofanyika kituo kikuu cha mabasi Ubungo jijini Dar-es-Salaam, Agosti 25, 2015.

Mkuu wa Timu ya Vijana- TAKUKURU Makao Makuu Bi.Dorothea Mrema alisema:

 • Kura ina thamani kubwa kwani bila ya wananchi kupiga kura ni vigumu wagombea kuweza kuchaguliwa.
 • Wagombea wanafahamu thamani ya kura ndiyo maana baadhi yao hutumia mbinu yoyote ikiwemo kutoa rushwa ili kuhakikisha wanapata kura kwani ndicho kipimo cha wao kuingia madarakani.
 • Vijana hawana budi kutambua thamani ya kura zao kwa kumchagua kiongozi bora ambaye atamtumikia kwa kipindi cha miaka 5. Kiongozi atakayejali maslahi ya wananchi na kutatua kero zao.

Katika kusisitiza hayo, Mwakilishi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bi.Miriam Mwendamseke aliwaasa vijana kuwa makini na ahadi za wagombea kwani viongozi watakao patikana kwa njia ya rushwa hawataweza kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya, shule, barabara, maji, na mengineyo. Alisema, Viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa hutumia muda wa uongozi wao kurejesha fedha zao na sio kuleta maendeleo kwa wananchi.

Wito ulitolewa kwa vijana kwa kuwataka wawafichue na kuwasilisha taarifa TAKUKURU za wale wote watakao jaribu kuwarubuni kwa njia ya rushwa ili wawachague. Ofisi za TAKUKURU zipo katika kila mkoa na kila wilaya nchi nzima.

Subcategories