JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Walionunua magari ya mitumba ATCL watiwa hatiani

                                                                                                        

 

 WALIONUNUA MAGARI MITUMBA ATCL WATIWA HATIANI                                

Na Mussa Misalaba

 

Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka, na  aliyekuwa Kaimu ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa ATCL, Elisaph Mathew, wamehukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh.milioni 70 au kwenda jela miaka 12 na kuilipa fidia ATCL jumla ya dola za Marekani 143,442.75 walizoisababishia hasara.

 Hukumu hii ilisomwa Septemba 13, 2017 na Hakimu  Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam,Victoria Nongwa,  aliyesikiliza kesi hii iliyokuwa na washtakiwa watatu.

 Mshtakiwa mwingine katika kesi hii alikuwa  aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani za ATCL, William Haji, ambaye aliachiwa huru na mahakama baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yake.

 Upande wa Mashtaka uliongozwa na Mwendesha Mashtaka toka ofisi ya Mkurugenzi wa  Mashtaka wa Serikali (DPP), Oswald Tibabyemya akisaidiwa na waendesha mashtaka  Shadrack Kimaro toka ofisi ya DPP; Moza Kasubi na Lizy Kiwia toka TAKUKURU.

 Katika kesi hii washtakiwa walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea ambapo Peter Swai alimtetea David Mattaka, Francis Mgale alimtetea Elisaph Mathew na Alex Mgongolwa alimtetea William Haji.

 Hakimu Nongwa alisema, mahakama baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 14 wa upande wa mashtaka iliona haukumgusa aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani za ATCL, William Haji.

 ‘Mahakama hii inamwachia huru Haji kwa sababu hakuna ushahidi unaomgusa dhidi ya tuhuma hizi. Mahakama inawatia hatiani washtakiwa wawili Mattaka na Mathew dhidi ya mashtaka yote sita”, alisema hakimu Nongwa.

 Mattaka na Mathew walitiwa hatiani na mahakama katika shtaka la kula njama kutenda kosa, mashtaka manne ya matumizi mabaya ya mamlaka na moja la kuisababishia hasara ATCL Dola za Marekani jumla ya 143,442.75.

Katika shtaka la kula njama kutenda kosa, mahakama iliamuru kila mshtakiwa alipe faini ya Sh.milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

 Katika mashtaka manne ya matumizi mabaya ya mamlaka, kila mshtakiwa aliamuriwa kulipa faini ya Sh.milioni tano kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.

 Katika shtaka la kusababisha hasara, mahakama iliamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh.milioni 10 au kutumikia kifungo cha miaka sita jela.

 Aidha, mahakama iliamuru vifungo kutumikiwa kwa pamoja ambapo kila mshtakiwa aliamuriwa kulipa faini jumla ya Sh.milioni 35 au kutumikia kifungo cha miaka sita jela

 Mbali na washtakiwa kutakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 35 au kutumikia kifungo cha miaka sita jela kila mmoja, mahakama iliwaamuru kuilipa fidia ATCL katika kipindi cha mwezi mmoja jumla ya Dola za Marekani 143,442.75 kutokana na hasara waliyoisababishia.

 Kabla ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka haukuwa na kumbu kumbu za makosa mengine dhidi ya washtakiwa na aliiomba mahakama itoe adhabu stahiki kulingana na makosa waliyotenda.

 Aidha, kabla ya hukumu kutolewa washtakiwa walipewa nafasi kujitetea ili wapunguziwe adhabu ambapo Mattaka aliiambia kuwa anashukuru imeona wema wake alioitendea ATCL mpaka walipo sasa.

‘Taarifa niliyonayo magari niliyoyanunua mpaka sasa yanatumika na ATCL haijaweza kununua magari mengine.Mimi nilikuwa nanusuru shirika kwa kutekeleza maagizo ya bodi’, alieleza Mattaka mbele ya mahakama.

 "Kwa sasa nina miaka 66 naelekea 67, ninasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu,ninamke na watoto na mama yangu ni mzee wa miaka 85. Mahakama iangalie na inionee huruma kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza”,alidai zaidi Mattaka.

Kwa upande wake Mathew alidai kuwa ni askofu anayewahubiria watu neno la Mungu, ni mkosaji wa mara ya kwanza, ana mke na watoto watatu, analea  watoto yatima watatu na anajukumu la kumlea mama yake mzazi ambaye amefiwa na mume wake.

 Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza mahakama yake itatoa adhabu kwa kuzingatia adhabu mbadala ikiwemo faini ama kifungo jela na akaongeza kuwa pamoja na mshtakiwa wa pili kuwa ni muhubiri na anayetoa huduma za kiroho, sheria lazima ichukue mkondo wake.   

                                       

Katika kutekeleza amri ya mahakama Mathew, ambaye kwa sasa ni Askofu wa kanisa la Pentekosti Motomoto alilipa faini ya Sh.milioni 35 Septemba 13 mwaka huu muda mfupi baada ya hukumu kutolewa na hivyo kujinasua kutumikia kifungo cha miaka sita jela.

 Hadi Septemba 19 mwaka huu Mattaka alikuwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka sita kwa kuwa baada ya hukumu kutolewa na mahakama hakuweza kulipa faini ya Sh. Milioni 35.

                                                          

Novemba 22, 2011 washtakiwa walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka sita ambapo moja  linahusu  kula njama kutenda kosa,  manne ya matumizi mabaya ya mamlaka na moja la kuisababishia hasara ATCL Dola za Marekani jumla ya 143,442.75 kutokana na manunuzi ya magari 26 yaliyotumika kinyume cha sheria , kanuni na taratibu. 

 

Kati ya Juni 2007 na Julai 2007 washtakiwa wakiwa waajiriwa wa ATCL walikula njama na  kutumia vibaya mamlaka yao kwa kununua magari 26 yaliyotumika toka kampuni ya uuzaji  magari ya Bin Dalmouk ya Dubai, Falme za Kiarabu,  kwa ajili ya matumizi ya ATCL bila ya kuwa kwenye bajeti ya Shirika.

 

Mbali na kununua magari yaliyotumika washtakiwa walikiuka Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa, hawakufuata taratibu za sheria ya manunuzi ya Umma na kanuni zake na walilisababishia Shirika hasara ya Dola za Marekani jumla ya 143,442.75 ikiwa ni gharama za kuhifadhi magari bandarini muda mrefu.