JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Jumuia ya Madola ni ushirikiano  wa hiari wa nchi zilizo na mamlaka sawa ya kiutawala zilizoungana kushughulikia mambo kadhaa ya muhimu ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa. Malkia Elizabethi 11 ndiye Mkuu wa Jumuia ya Madola. Sekeritariati ya Jumuia ya Madola ndiyo  hushughulika na uendeshaji wa shughuli za Jumuia siku hadi  siku na inaongozwa na Katibu Mkuu ambaye huchaguliwa na wanachama wa Jumuia ya Madola. Makao makuu ya Jumuia ya Madola yako Marlborough, Uingereza. Masharti ya kujiunga na Jumuia ya Madola ni pamoja na kwamba nchi iwe imewahi kutawaliwa na Uingereza moja kwa moja au kwa namna nyingine, au nchi iwe na uhusiano  wa kiutawala na nchi ya Jumuia ya Madola, au nchi iwe tayari kufuata kanuni , misingi na vipaumbele vya Jumuia ya Madola vilivyoainishwa katika tamko la Harare la mwaka 1991 na pia nchi iwe tayari kukubaliana na kanuni na mapatano ya Jumuia ya Madola. Hadi sasa Jumuia ina  wanachama wapatao 53 . Nchi za Jumuia ya Madola ziko Afrika, Amerika, Ulaya na Pacifiki lakini  zinatofautiana kwa maana kwamba zipo zilizo kubwa, ndogo, tajiri na masikini. Nchi 32 ni Jamhuri, 5 ni falme na 16 zinaongozwa na Mawaziri wakuu ambao wanawajibika kwa Malkia wa Uingereza. Jumuia ya Madola haina katiba na hujiendesha kwa kufuata taratibu zinazofahamika, mazoea na matamko mbalimbali au utayari wa kufanya jambo. Mashauriano baina ya serikali ndiyo chanzo cha welekeo katika ushirikiano.Maadili na misingi ya Jumuia ya Madola imefafanuliwa katika Mwongozo wa Jumuia ya Madola(Charter of Commonweallth) uliotolewa na kuanza kutumika mwaka 2013.

Jumuia ya Madola ina amini kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo iko salama kutokana na madhara ya rushwa. Rushwa inauwezo wa kuathiri nchi zilizo na utajiri wa raslimali, zinazoendelea, na zenye uchumi ulioendelea. Rushwa inaathiri utawala wa sheria, maendeleo na ukuaji wa uchumi.Kwa zaidi ya miongo miwili Jumuia ya Madola imekoa ikitoa msaada kwa serikali wanachama katika kukabiliana na rushwa kwa kubadilishana uzoefu, mafunzo na kujenga uwezo na  utafiti wa sera. Jumuia ya Madola inazisaidia serikali na mamlaka zake namna ya kutengeneza na kutekeleza mikakati ya kupambana na rushwa kwa kushirikiana na taasissi zisizo za kiserikali na wafanyabiashara. Nchi wanachama husaidiwa na mtandao wa zaidi ya 80 unaohusisha taasisi zisizo za kiiserikali, taasisi za kitaaluma na kitamaduni na taasisi za kiserikali. Jumuia ya Madola inayo Sekeretariati ambayo  hutoa mwongozo kuhusiana na masuala ya utungaji wa sera, misaada ya kiufundi, na huduma za kiushauri kwa nchi wanachama. Maeneo ya kupambana na rushwa ni pamoja na kuimarisha utawala na sekta ya umma, kuimarisha utawala wa sheria, kuimarisha uwazi katika matumizi ya maliasili, na kusaidia uadilifu katika michezo.

Kituo cha kupambana na rushwa cha  nchi za jumuia ya madola Afrika ( Commonwealth Africa Anti- Corruption Centre – CAACC)

Kituo cha kupambana na rushwa cha nchi za jumuia ya Madola Afrika  kiko Gaborone Botswana.Kituo hiki kilianzishwa na Sekeritariati ya Jumuia ya Madola kwa ushiririkiano na serikali ya Botswana na Umoja wa Mamlaka za  Kupambana na Rushwa wa Jumuia ya Madola Afrika mwezi  Februari 2013. Ni taasisi isiyo na nia ya kupata faida katika shughuli zake.Wanachama wake ni Mamlaka zote 18 za Kupambana na Rushwa Afrika. Kituo hicho hutoa mafunzo,uendelelezaji na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uchunguzi, utafiti, elimu kwa umma, kuzuia, uchunguzi wa kitaalam, uongozi na utawala, maadili ya kazi, uendeshaji wa mashtaka, ufuatiliaji wa mali, ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za mapambano dhidi ya rushwa, mipango ya kitaalamu pamoja na kujenga uwezo wa kimaendeleo katika kupambana na rushwa  kwa nchi wanachama na maofisa. Kituo kimefanya kazi na mashirika kama vile UNDP, Transparency International na shirika la umoja wa mataifa,  ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC). Kwa msaada wa shirika la kimataifa la uwazi kwa mfano, kituo kimeanzisha dawati la msaada ili kuzisaidia taasisi wanachama wa kupambana na rushwa huduma ya kitalaam na  utafiti kwa  haraka.