JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Robert Rwezaura, Ngorongoro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ngorongoro imeokoa zaidi ya shilingi milioni 6 kutokana na malipo ya mishahara hewa kwa watumishi waliofukuzwa kazi katika hospitali ya Wasso iliyopo Ngorongoro Machi 22, 2017.

Awali katika shauri hilo Hospitali ya Wasso ilipokea Shilingi 2,481,301 kama mishahara ya watumishi wawili ambao tayari walishaachishwa kazi na uongozi wa Hospitali hiyo lakini bado mishahara hiyo iliendelea kupokelewa hospitalini hapo bila kurejeshwa hazina kama mishahara hewa kwa watumishi ambao hawapo kazini.

Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Ngorongoro baada ya kupata taarifa hizo ilianza kufanya uchunguzi na kubaini kuwa Hospitali ya Wasso iliendelea kupokea mishahara kutoka serikalini ya watumishi ambao ilikwisha waachisha kazi bila kuzirejesha hazina.

Aidha, TAKUKURU ilibaini kuwa Bw.Julius Ole Sitoy awali alikuwa mtumishi wa hospitali ya Wasso akiwa kama mlinzi wa hospitali hiyo  na baadae kufukuzwa kazi  Aprili 13, 2015 lakini bado aliendelea kupokea mshahara tangu Mei, 2015 hadi Machi 2016 akilipwa jumla ya kiasi cha Tshs.1,426,812 kinyume taratibu za utumishi wa umma kwa mtu aliyefukuzwa kazi.

Pia TAKUKURU ilibaini kuwa Bw. Daudi Salya Nambololo ambaye nae alikuwa mtumishi wa Hospitali ya Wasso Hospital katika kituo cha Digodigo kama mlinzi, aliachishwa kazi   Septemba 25, 2015 lakini Pamoja na kuachishwa kazi bado ailiendelea kulipwa mshahara  kutoka serikalini kuanzia  Oktoba 2015 hadi Machi 2106 yenye jumla ya Tshs.1,054,489

Baada ya uchunguzi kufanyika na kufanya mahojiano na Hospital ya Wasso walikubali kufanyika kwa makosa hayo na kuanza kurejesha pesa yote iliyokuwa imelipwa kimakosa  kiasi Tshs.2,481,301 walichokuwa wamekipokea kutoka serikalini kama mishahara ya watumishi wawili waliokuwa wameachishwa kazi.

Aidha, pesa hiyo ilirejeshwa kwa katibu Mkuu Hazina kupitia CSP Misc.Deposit,Bank of Tanzania akaunti namba 9921167201 Dar-es-Salaam kwa hundi namba 065023 ya             Januari 11, 2017 kupitia Fund Transfer Request Form namba 0931185.

Wakati huohuo Bw. Nehemia Mshote fundi sanifu maabara katika Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mnamo Julai 15, 2015 kwa ridhaa yake mwenyewe aliamua kuacha kazi kwa kuandika barua ya masaa 28, lakini bado aliendelea kupokea mishahara kupitia katika akaunti yake namba 41110001166 iliyopo benki ya NMB tawi la Loliondo jumla ya kiasi cha        Tshs.4, 925,000.

Aidha, Baada ya ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro kufanya uchunguzi mtuhumiwa na kulifatilia kwa karibu swala hilo Bw.Nehemia Mshote aliamua kurejesha kiasi cha         Tshs.4, 182,000/= kati ya Tshs.4, 925,000/= alizochukua.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) imemfikisha  mahakamani ofisa forodha msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye kituo chake cha kazi ni Mapato House, Jenifer Emanuel Mushi, kwa makosa mawili ya rushwa.

Mshtakiwa alipandishwa kizimbani Oktoba 24, 2017 na kusomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Vitalis Peter, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30, 2016 mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa umma alitenda kosa la kupatikana akimiliki magari 18 yenye thamani ya Shilingi 197,601, 207/= ambayo hailingani na mapato yake halali kinyume na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kosa la pili linalomkabili ni kuwa kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016 akiwa mwajiriwa wa umma aliishi kiwango cha maisha kinachofikia Shilingi 333,255,556.24 ambacho hakilingani na mapato yake halali kinyume na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. 

Mshtakiwa alikana mashtaka dhidi yake na upande wa mashtaka uliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ambayo ingeona inafaa kwa ajili ya usikilizaji wa hoja za awali kwa kuwa uchunguzi wa shaauri umekamilika.

Mshtakiwa kupitia kwa wakili wake wa kujitegemea, Elisalia Mosha, aliiomba mahakama kumpaitia dhamana kwa sababu mashtaka dhidi yake yanadhaminika kisheria.

Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalikuwa ni kuwa na mdhamini mmoja ambaye alitakiwa kusaini bondi ya Shilingi milioni 20 na kesi imeahirishwa hadi Novemba 7 mwaka huu itakapokuja kwa usikilizaji wa hoja za awali.

 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imemhukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya TSh.1.5000,000/= aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Johanes Monyo, baada ya kumkuta na hatia ya kosa la kutumia vibaya mamlaka yake kwa  kutoa ajira kwa Chacha Wambura kinyume na sheria za utumishi wa Umma.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama tarehe 15/11/2016 mbele ya Hakimu Mfawidhi Mheshimiwa Agustino Rwezile katika shtaka la Jinai namba 18/2015 lililokuwa linaendeshwa na waendesha mashtaka wa TAKUKURU Violet Machary, Monica Kijazi na Hamidu Simbano.

Mshtakiwa alikutwa na hatia na mahakama katika kosa  la kutangaza  na kuajiri nafasi ya Afisa Raslimali Watu bila ya kuwa na kibali cha Idara ya Utumishi kinyume na Kifungu cha 29(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8/2007 kitendo kilichopelekea Chacha Wambura kujipatia manufaa ya ajira na mshahara asiostahili.

Mshtakiwa alilipa faini ya TSh.1, 500,000/= na kujinasua kwenda kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela katika gereza la Kisongo, Arusha.