JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Geita leo tarehe 04/02/2019 imemtia hatiani Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Interlands Surveyors Co. Ltd Ndg. RENATUS KASOGOTI MOGOSU kwa kosa la kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 katika Shauri Na 03/2017 alilokuwa anakabiliana nalo hapo mahakamani.

 Mshitakiwa huyo alitiwa hatiani na Mhe Hakimu Jovith Kato ambaye alieleza kuwa mahakama imezingatia ushahidi wa Jamuhuri na ushahidi wa utetenzi na hatimaye kufikia maamuzi ya kumtia hatiani Mshitakiwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri ya kwamba haukuacha shaka lolote.

Awali ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU Ndg. Dennis J. Lekayo kuwa  mnamo tarehe 22/11/2011 Mshitakiwa kwa niaba ya Kampuni yake aliingia Mkataba Na. LGA/091/IFP/PS/2011/2012/4 na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupima viwanja 2,000 katika eneo la Magogo Wilayani humo. Aidha upande wa mashitaka uliwasilisha ushahidi kuwa mnamo tarehe 28/07/2012 Mshitakiwa aliwasilisha madai ndani yake akieleza kuwa viwanja 2,000 vimepimwa kama mkataba ulivyotaka na kwa mantiki hiyo aliwasilisha Hati ya Madai Na. 12/46 ya tarehe 28/07/2012 ili kulipwa fedha kwa mjibu wa mkataba huku akijua kuwa taarifa hiyo haikuwa ya ukweli na ililenga Kumdanganya Mwajiri ambaye ni Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

 Kwa mjibu wa uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ilibainika kuwa vilipimwa viwanja 1,607 badala ya viwanja 2,000  lakini kutokana na taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mshitakiwa pamoja na Hati ya Madai Halimashauri ya Wilaya ya Geita ililipa fedha zote zikiwemo TZS. 43,230,000/= ambazo ni thamani ya wiwanja 393 hambavyo havikupimwa na malipo hayo hayakusitahili kulipwa kwa Kampuni hiyo ya Mshitakiwa. 

 Baada ya kubaini hivyo TAKUKURU ilimfungulia mashitaka Mshitakiwa ya Kutumia nyaraka Kumdanganya Mwajiri kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/20007 na Kuisababishia Serikali hasara ya TZS. 43,230,000/= kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Mapitio ya 2002 lakini Mahakama haikumkuta na hatia juu ya kosa hilo baada ya kubaini kuwa Kampuni ya Mshitakiwa baada ya kujulishwa mapungufu hayo ilifanya upimaji katika eno la Mpunvu kufidia viwanja 393 alivyo lipwa bila kupimwa.  

 Baada ya kujiridhisha na ushahidi na hoja zilizotolewa na Jamuhuri, Mahakama ilimtia hatiani Renatus Kasogoti Magoso kwa kosa la Kutumia Nyaraka na kuamuru alipe faini ya TZS. 500,000/- au kwenda Jela miaka 3.  Mshitakiwa alifanikiwa kulipa faini hiyo kama ilivyoamuliwa na Mahakama.  

 Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Geita Bw. THOBIAS NDARO anatoa wito kwa wananchi  wote wa mkoa wa Geita kuendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa kwa maendeleo ya mkoa na nchi yetu.

 

 Imetolewa na Thobias Ndaro - Mkuu wa TAKUKURU (M) Geita