JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

RPC Geita awataka Polisi kuzingatia sheria na kutojihusisha na rushwa

Na Juntwa Mwakujonga, Geita

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Geita, SACP Ladson Mwabulambo Mponjoli amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi ya Jeshi hilo na kutojihusisha na vitendo vya rushwa wanapotekeleza majukumu yao.  Wito huo aliutoa wakati wa semina iliyofanyika katika bwalo la Polisi Geita  Februari 23, 2017.

Akifungua semina hiyo, SACP Mponjoli  aliwaeleza washiriki hao kuwa wao ni  watumishi kama watumishi wengine wa umma na akawataka kuzingatia kanuni na mwongozo wa Jeshi la Polisi katika  kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu. Aliwaasa pia kudumisha nidhamu na utii kama ulivyo utamaduni wa Jeshi hilo.

Jeshi la Polisi ni mdau mmojawapo katika mapambano dhidi ya rushwa hivyo tuna wajibu wa kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa na kwa ushirikiano huo tutafanikiwa kulimaliza tatizo hili  nchini,” alisema Kamanda Mponjoli.

Mada kuu katika semina hiyo iliyowashirikisha askari 81 ilikuwa “Wajibu wa Askari wa Jeshi la Polisi katika Mapambano dhidi ya Rushwa.”   Semina hiyo ni utaratibu wa Jeshi hilo mkoani Geita kutoa mafunzo mbalimbali kwa askari polisi kila alhamisi ili kuwakumbusha wajibu wao katika kazi.

Akiwasilisha mada hiyo, Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita, Bw. Hajinas Onesphory alibainisha kuwa wananchi wanalilalamikia Jeshi hilo kwa mambo mengi ikiwemo kunyimwa fursa ya kuwadhamini ndugu zao wanapowekwa mahabusu. Alifafanua kwamba wananchi wanatoa mfano wa usemi “kuingia bure ila kutoka kwa pesa” kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi na kinachorudisha nyuma vita dhidi ya rushwa.

Bw. Onesphory alisema malalamiko mengine yanahusu askari wa usalalama barabarani ambao wanatuhumiwa kuwashawishi wananchi wanaovunja Sheria ya Usalama Barabarani iliyoboreshwa mwaka 2002 kuwapatia rushwa ili wasichukuliwe hatua za kisheria. Wananchi hao pia wanalalamikia kitendo cha  kuombwa pesa ya mafuta ya gari la Polisi ili kwenda kushughulikia tukio la uhalifu au wanapohitaji msaada kutoka Jeshi hilo.

Akijibu baadhi ya malalamiko hayo, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, ASP Julius Masanyiwa  alisema Jeshi la Polisi halina utaratibu wa kuwaomba watoa taarifa au waathirika wa matukio ya uhalifu pesa ya mafuta ya magari bali ni jukumu lao kuhakikisha wanapata mafuta ya kuwawezesha kufika kwenye matukio ya kihalifu. Alishauri kuwa mwananchi  akiombwa fedha ya mafuta na askari yeyote asisite kutoa taarifa ngazi za juu ili taratibu za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya askari huyo.

Naye Bw. Juntwa Mwakujonga aliyeambatana na Bw. Onesphory, aliwakumbusha washiriki kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria wakiwemo Askari Polisi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Bw. Mwakujonga pia aliwaasa askari hao kutosheka na vipato vyao kwani baadhi ya watumishi huwa hawaridhiki na vipato hivyo na kutaka kuongezewa mshahara. Aliwaambia kuwa mshahara mdogo kisiwe kisingizio cha kujihusisha na vitendo vya rushwa.