JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Brigedia Generali John Julius Mbungo akila kiapo mbele ya Rais Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli alimwapisha Brigedia Generali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Agosti 24, 2017.

Brigedia Generali John Julius Mbungo aliapishwa katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ambao ni pamoja na  Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi na Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Harold Nsekela.

 Mbali na viongozi wa Serikali, viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama toka Jeshi la Ulinzi na Usalama, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji , Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na TAKUKURU nao walihudhuria hafla hii.

Mbali na kula kiapo cha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Generali John Julius Mbungo alikula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Mhe. Harold Nsekela kwa kuzingatia misingi ya maadili iliyoainishwa katika Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, ambayo yanamtaka kila kiongozi wa umma kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kuhusu utendaji wa Serikali;

Akizungumza mara baada ya kumwapisha Brigedia Generali John Julius Mbungo Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuli alimpongeza Brigedia Generali Mbungo kwa kushika nafasi hii nyeti ambayo mbali na kusema ana imani naye kuwa atatekeleza majukumu yake kwa uadilifu mkubwa alisema ilimchukua muda mrefu  kumpata kiongozi sahihi wa kukamilisha  safu nzuri ya uongozi TAKUKURU.

Mhe. Rais aliipongeza TAKUKURU kwa kuonyesha mafanikio katika vita dhidi ya rushwa lakini aliitaka  kuongeza juhudi zaidi katika uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka ili wala rushwa wengi zaidi washughulikiwe kwa wakati na bila kumwogopa mtu yeyote ili ifike mahali tuseme Tanzania bila rushwa inawezekana.

Mhe. Rais aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa  katika kila sekita  ili wafadhili waendelee kuwa na imani na Serikali ya Tanzania ambao kwa hivi sasa wameanza kurudisha misaada baada ya kuona  jitihada nzuri za serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.

Aidha, Mhe. Rais alimwagiza Kamishina wa Sekeritarieti ya Maadili ya Viongozi  wa Umma Jaji Mstaafu Mhe. Harold Nsekela apitie sheria ya maadili ya viongozi wa Umma na kuwasilisha serikalini mapungufu yaliyopo ili sheria ifanyiwe marekebisho mapema iwezekanavyo.

Kabla ya Mhe. Rais kuzungumza, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Generali John Julius Mbungo, alimshukuru Rais kwa kumwamini na kumteua kwa nafasi hii na alimwahidi kuwa atatekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa mujibu wa sheria na kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkuu, wakurugenzi na watumishi wote wa TAKUKURU kwa ujumla na wadau wote wa mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa upande wake Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Harold Nsekela, aliwakumbusha viongozi wa Umma kuwa wanajukumu la kujaza fomu za tamko la mali na madeni kwa wakati na kikamilifu na wawe tayari kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pale  inapofanya uhakiki wa mali zao na madeni yao.

Aidha, Mhe. Nsekela alieleza kuwa kwa sasa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina mapungufu makubwa kwa vile inatoa adhabu ndogo sana kwa viongozi wanaoikiuka na wengi wa viongozi wamekuwa hawatilii maanani matakwa ya sheria hii ambapo wamekuwa wakijaza fomu za tamko la mali na madeni dakika za mwisho na hawasemi ukweli.

Pia, Mhe. Nsekela alisema watapitia matamko ya mali na madeni ya viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kurudi nyuma ili waone hali halisi ya uadilifu wa viongozi wa umma.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki alimshukuru Rais kwa kumteua Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Generali John Julius Mbungo, kwa kuwa nafasi hii ilikuwa wazi kwa muda mrefu.

Mhe. Angela Kairuki pia alimhakikishia Rais kuwa atashirikiana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Generali John Julius Mbungo, ili kufanya kazi kwa kasi na haki bila kumwonea mtu na aliwaomba wananchi waendelee kushirikiana na TAKUKURU ili iwe na tija katika utumishi wa Umma.

Hali kadhalika, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Alex Mfungo alimpongeza Rais kwa kumteua Brigedia Generali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na alimwahidi kuwa viongozi  na watumishi wa TAKUKURU  kwa ujumla watashrikiana naye na hawatamwangusha.

Nafasi ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ilikuwa wazi tangu Desemba 16, 2015 baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, kuteuliwa na Rais kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu iliyokuwa wazi kufuatia Mhe. Rais kutengua uteuzi wa Dr Edward Hosea.

Kabla ya uteuzi huu Brigedia Jenerali John Julius Mbungo alikuwa Mkuu wa tawi la Huduma za Sheria  na pia Kaimu Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) .

Brigedia Jenerali John Julius Mbungo ana shahada ya kwanza ya sheria (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na Shahada ya pili katika masuala ya Haki za Kimataifa za binadamu (Chuo Kikuu cha Birmigham).

Aidha, Brigedia Jenerali John Julius Mbungo ni Wakili wa Mahakama kuu isipokuwa Mahakama ya Mwanzo.