JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

P.O.BOX 1020

Tabora

Mkoa: Tabora

Simu: (026) 2604030 / 2604311

Fax (026) 2604039

Barua pepe: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Tovuti: www.pccb.go.tz

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tabora, imewapandisha kizimbani na kuwafungulia Kesi ya Jinai Na. 14/2019 wafanyakazi wawili wa Shirika la Umeme (TANESCO) Wilaya ya Uyui ndugu Daudi Filbert Mwiru (28) ambaye ni Fundi Sanifu na Maulidi Amani Maulidi (29) ambaye alikuwa Fundi Msaidizi Kibarua kwa makosa ya kushawishi na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu cha 15(1) a na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora tarehe 1 Februari, 2019 kujibu mashitaka yanayowakabili.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Mheshimiwa Ajali Toma Milanzi, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Mashingia Simoni aliieleza Mahakama kuwa Mwezi Disemba, 2018 washtakiwa walishawishi hongo ya Shilingi laki mbili (200,000/=) toka kwa Kimwaga Mfutakamba mkazi wa Goweko ili wasiondoke na Mita ya umeme aliyokuwa ameihamisha na kuiunganisha katika nyumba nyingine kinyume na utaratibu.

Mashingia Simoni alisema tarehe 7, Disemba 2018 mshtakiwa Daudi Filbert Mwiru alipokea kiasi cha Shilingi laki moja na elfu ishirini na tano (125,000/=) toka kwa Venant Protas ambaye ni ndugu wa Kimwaga Mfutakamba ikiwa ni malipo ya awali ambapo walirejesha Mita hiyo pasipo kuunganisha umeme hadi hapo watakapomalizia kiasi kilichosalia cha tshs.75,000=

Katika Shitaka lingine, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Mashingia Simoni aliieleza Mahakama kuwa Mwezi Disemba, 2018 mshtakiwa Daud Filbert Mwiru alishawishi na kupokea shilingi laki moja (100,000/=) toka kwa Boniface Mpuzumbi mkazi wa Goweko wilayani Uyui na kurejesha Mita na umeme iliyokuwa ameiondoa baada ya mita hiyo kuhamishiwa na kuunganishwa katika nyumba ya mama yake Boniface Mpuzumbi kinyume na utaratibu, kazi ambayo ilifanywa na Kishoka.

Washtakiwa wote wawili walikana mashitaka yao na wapo nje kwa dhamana. Aidha upelelezi umekamilika na kesi hiyo itakuja tena mahakamani tarehe 28 februari, 2019 kwa ajili ya kusoma hoja za awali.

 

IMETOLEWA NA: MASHAURI ELISANTE, KAIMU MKUU WA TAKUKURU MKOA

04/02/2019